SOMO LA KWANZA: Mdo 2 :1-11
SOMO LA PILI:
1 Kor. 12 : 3-7, 12-13
INJILI ; Jn.
20 :19-23
Ndugu zangu katika Yesu Kristu leo tutafakari historia ya sikukuu ya Pentekosti, umuhimu wa Roho Mtakatifu katika maisha ya Mitume na hatimaye kile tunachoweza kujifunza kutokana na sikukuu ya leo. Kwa Wakristo Pentekosti ni ishara ya kukamilika kwa msimu wa pasaka na malengo yake. Ni siku ya kuzaliwa kwa Kanisa. Lakini ni muhimu kujua kwamba neno Pentekosti linamaanisha "hamsini au ya hamsini." Pentekosti hapo awali ilikuwa sikukuu ya mavuno kwa Wayahudi. Wayahudi walikuwa wakisherehekea sikukuu ya mavuno baada ya siku ya hamsini ya sikukuu ya Pasaka. Wakati Mungu alipowaachilia Waisraeli kutoka utumwani na kuwaongoza kuingia katika Ardhi ya Ahadi, Bwana aliwabariki kwa ardhi nzuri na baadaye kila mwaka wakati wa mavuno yao ya kwanza, Waisraeli walipaswa kuwa ya sikukuu na kumshukuru Bwana. Walipaswa kukumbuka jinsi Mungu alivyowatoa katika utumwa huko Misiri na kuwaleta katika Nchi ya Ahadi, ambako wangefurahiya fadhila kama hiyo. Pili, baadaye wakati wa sikukuu hii pia walikumbuka agano la Mungu alilofanya na Waisraeli, "Mimi ni Mungu wako, na ninyi ni watu wangu." Ilikuwa tu sherehe ya Kiyahudi. Sasa ikawaje iwe sikukuu ya Kikristo? Kuna sababu mbili. 1. Kwa sababu baada ya majuma saba ya ufufuo wa Yesu, Roho Mtakatifu alimwagwa juu ya wale wafuasi wa Yesu ambao walikuwa wamekusanyika pamoja huko Yerusalemu na watu wengi wakawa Wakristo. Hayakuwa mavuno ya ngano tena bali mavuno ya watu ambao wakawa Wakristo. 2. Baada ya miaka kadhaa ya ufufuo wa Yesu, Wakristo wa kwanza walipokumbuka asili yao walichagua sikukuu hii kuashiria kuzaliwa kwa agano jipya la Mungu na watu wake.
Je! Roho Mtakatifu alikuwa na umuhimu gani katika maisha ya Mitume na kwa Kanisa? Kabla ya Yesu kupaa mbinguni, anawatuma wanafunzi wake kuwa mashuhuda wake huko Yerusalemu, Yudea, Samaria hadi miisho ya ulimwengu. Lakini mara tu Yesu alipoaacha walikaa kwenye vyumba vyao vya juu na kujificha. Waliogopa Wayahudi. Walijua kuwa watu hawawapendi, walijua kuwa mafundisho yao yalikuwa tofauti na ujumbe wa Wayahudi, na walitamani kujificha wenyewe vitandani ili wasionekane kwa wanajamii waliowachukia. Lakini nguvu ya Roho Mtakatifu iliwapa ujasiri wa kutoa maisha yao kwa Yesu kuwa washuhuda wake na kueneza habari njema ya upendo wa Mungu kwa wanadamu wote. Wakati hofu ya maisha ilipoipooza Imani yao kiasi cha kukata tamaa, Roho Mtakatifu aliwaamsha na kuwapa nguvu ya kutoka nje walikojificha na kuwafanya wa tofaauti. Roho Mtakatifu aliwakumbusha kama wana utume. Dhamira yao ilikuwa kuvunja kuta za chuki, mgawanyiko, na ubinafsi. Hili liliwezekana kwa kuptia msaada wa Roho Mtakatifu.
Sasa ni nini maana ya sikukuu ya Pentekosti katika maisha yetu? Siku ya Pentekosti imewekwa kwa ujasiri na wingi. Ni wakati wa kufurahi, wakati wa kukumbuka na wakati wa kufurahi katika yale ambayo Bwana amefanya maishani mwetu. Katika nyakati za giza, tunapokuwa na wasiwasi juu ya maisha yetu ya baadaye, na mustakabali wa watoto wetu, wakati nguvu za uovu zinaonekana kuongezeka kuliko wema, wakati tunapokuwa katika hatua ya kukata tamaa maishani, wakati maisha yetu yanapoonekana kuwa ya zamani na yamechoka na kuchokea , Pentekosti inaibuka katika maisha yetu tena na inatukumbusha, kwamba sisi ni sehemu ya mavuno ya matunda yaliyopandwa na Kristo na yaliyowezekana kwa dhabihu yake. Na hiyo, inabadilisha kila kitu!
Hapo kale, palikuwa na mvulana aliyeitwa Olu ambaye alikuwa na kuku mweupe aliyempenda sana. Walikuwa marafiki wakubwa walioishi pamoja na wala hawakuweza kutenganishwa. Siku moja, kuku yule alitoweka, Olu alilia sana. Halafu baada ya wiki tatu, kuku mweupe alirudi akiwa na vifaranga saba weupe na wazuri. Olu alikuwa tena na furaha kubwa isiyo na kifani. Mama kuku aliwatunza vifaranga wale kwa uangalifu mkubwa. Siku moja, mwishoni mwa kiangazi, vijana Fulani walichoma moto kuzunguka eneo la kichaka kilichokuwa nje ya kijiji. Madhumuni yao yalikuwa kuwakimbiza wanyama wadogo kama vile sungura na swala waliokuwa wamejificha humo. Hapo yale mapanga yakawashambulia wanyama hao. Wakati wa mawindo kukamilika na moto kufifia, Olu na marafiki zake walitembea juu ya majivu yaliyokuwa bado yanafuka moshi. Olu aligundua rundo la manyoyo na kuhisi harufu ya nyama iliyoungua. Lilionekana kama masalia ya ndege ambaye hakuweza kukimbia moto. Halafu Olu aligundua kwa huzuni. Alikuwa yule kipenzi chake, kuku mweupe, ambaye alikuwa ameungua na kuwa mkaa mweusi. Lakini ghafla akasikia sauti ya vifaranga. Mama Kuku alikuwa amewafunika kwa mwili wake na walikuwa hai na wazima kabisa. Mama kuku aliyatoa maisha yake kwa ajili ya watoto wake. Alikufa ili vifaranga wapate kuishi.
Pentekosti inatukumbusha kwamba wakati tu tunapofikiria kuwa hakuna tumaini katika maisha, wakati tunahisi kwamba hakuna dhamani ya maisha, kwa Roho Mtakatifu tunapata kutimizwa na kukamilika. Pentekosti sio msimu tu au sikukuu tu ya kila mwaka. Sio jambo au tukio ambalo tunakumbuka tu. Ni mwanzo wetu, ni lango la kuingilia, wakati wetu wa sasa. Roho Mtakatifu anaendelea kufanya kazi ndani yetu kutubadilisha na kutuhimiza, ili kazi kubwa ya wokovu ya Mungu iweze kuonyeshwa kwetu na kukamilishwa. Kwa Kuhamasishwa na tendo la Roho Mtakatifu, tunapokea ujasiri wa kuinua mioyo yetu kwa tumaini, na Roho hutujaza, kutufanya tuwe wapya. Kwa hivyo popote tulipo leo, katika hali yoyote tupitayo, tujue ya kuwa Roho yuko pamoja nasi. Kwa Kuhamasishwa na tendo la Roho Mtakatifu, tunapokea ujasiri wa kuinua mioyo yetu kwa tumaini, na kujazwa roho na kutufanya tuwe wapya.